Jumapili 15 Februari 2026 - 23:30
Vitisho vya Rais wa Marekani ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na uvamizi wa mamlaka ya Iran

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Abdallah Al-Daqqaq amesema; vitisho vya Rais wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ni “ukiukaji wa kanuni za kimataifa na uvamizi wa mamlaka ya nchi yenye nafasi ya kikanda na kidini”, akisisitiza kwamba kumlenga Kiongozi wa Mapinduzi ni kushambulia alama ya kisiasa na kidini iliyounganishwa na hisia za mamilioni ya Waislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, mkutano wa waandishi wa habari katika kuadhimisha kumbukumbu ya Mapinduzi ya Bahrain ulifanyika tarehe 25 Bahman katika Makumbusho ya “Pango la Ujasusi la Marekani”, ukihudhuriwa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Abdallah Al-Daqqaq, mwanazuoni wa kimapinduzi wa Bahrain na mwakilishi wa Sheikh Isa Qassim. Ujumbe wa Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa Mapinduzi ya Bahrain, ulisomwa katika hafla hiyo.

Al-Daqqaq akisisitiza kuwa; haki haipotei kwa kupita kwa muda, hasa inapokuwa na wadai wake, alisema: tarehe 14 Februari 2011 ilikuwa hatua muhimu katika historia ya kisiasa ya Bahrain — siku iliyoonesha kuwa wananchi wa Bahrain wanatafuta heshima ya kibinadamu na mabadiliko yatakayohakikisha haki za kijamii na kisiasa za raia wote kwa usawa.

Alisema kuwa; suala kuu la Bahrain ni madai ya wananchi ya uadilifu katika mustakabali wa kisiasa wa nchi, akiongeza kuwa wananchi wa Bahrain wameendelea kushikamana na madai yao halali, njia ya amani na mazungumzo ya umoja wa kitaifa, licha ya serikali kutumia “mbinu za kuondoa wapinzani na kulipiza kisiasa”.

Al-Daqqaq alisema; mamlaka za Bahrain zimejaribu kumaliza uwepo wa kisiasa na kidini wa wapinzani kupitia hatua za kiusalama, ikiwa ni pamoja na kuvunjwa kwa Baraza la Wanazuoni, chama cha Al-Wefaq, Jumuiya ya Uamsho wa Kiislamu na vyama vingine vya kisiasa, pamoja na kuwakamata viongozi wa upinzani.

Aliongeza kuwa; shinikizo lilifika hadi kwenye majukwaa ya kidini, ambapo Swala ya Ijumaa ya Sheikh Isa Qassim ilisimamishwa. Alisema, watawala wa Bahrain wanajaribu kutumia mimbar za dini kuhalalisha mradi wa kusawazisha uhusiano na Israel na kukubali sera za Marekani, lakini akasisitiza kuwa wananchi wa Bahrain hawatakubali kuuza dini yao.

Aidha, aliikosoa vikali sera rasmi  zilizohusisha kuvuliwa uraia mamia ya wananchi, utekelezaji wa hukumu za kifo na mamia ya kesi za mahakama zisizo za haki. Aliongeza kuwa; deni la serikali ya Bahrain limezidi dinari bilioni 20 (takriban dola bilioni 60), huku kukiwa na ukosefu wa uangalizi madhubuti wa matumizi. Alielezea kusawazisha uhusiano na Israel kuwa “hatari kubwa zaidi”, akisisitiza kuwa wananchi wa Bahrain hawatambui utawala huo.

Mwanazuoni huyo aliwauliza watawala wa nchi yake kwa kusema: “Miaka kumi na tano ya sera ya kiusalama na kupuuza madai ya wananchi imezaa matokeo gani?” Alisema nguvu ya dola ni kuwaunganisha raia wote chini ya mwavuli mmoja na kuwafanya wapinzani kuwa washirika katika kujenga mustakabali wa taifa, si kuwaadhibu kwa mbinu za kiusalama.

Alisisitiza kuwa; mzizi wa mgogoro wa Bahrain ni wa kisiasa, na kwamba matatizo ya haki za kiraia, uchumi na vikwazo vingine vinatokana na hilo. Alitoa wito wa kuandikwa katiba inayokubaliwa na wote — Shia na Sunni — ambapo wananchi wawe mhimili mkuu, badala ya katiba ya mwaka 2002.

Al-Daqqaq alisema kuwa; tangu mwaka 2011 hadi sasa takriban wananchi 20,000 wamekamatwa, na zaidi ya wafungwa 190 wa kisiasa bado wako gerezani. Aliziambia familia za wafungwa:
“Nyinyi ni heshima ya Umma, na subira yenu ni ishara ya kudumu kwa harakati hii.”

Alisisitiza kuwa; suala la wafungwa wa kisiasa si la kifamilia pekee bali ni la kitaifa, na wote wanapaswa kuachiliwa mara moja pamoja na kufidiwa madhara waliyopata.

Katika sehemu nyingine ya mkutano huo, Al-Daqqaq alirudia kusema kuwa; vitisho vya Rais wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na Kiongozi wa Mapinduzi ni ukiukaji wa kanuni za kimataifa. Alionya kuwa heshima ya pande zote ni sharti la mazungumzo ya kimataifa yaliyo sawa, na lugha ya vitisho huongeza mvutano huku ikiimarisha mshikamano wa kisiasa na wa wananchi.

Al-Daqqaq alisema sera za Washington zimechangia kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati na kusababisha gharama kubwa za kibinadamu na kiuchumi. Alitaja pia kesi ya “Jeffrey Epstein” kama mfano wa mgogoro wa maadili na sheria katika jamii za Magharibi.

Alimalizia kwa kusema kuwa; suala la Bahrain litaendelea kujadiliwa katika majukwaa ya kimataifa, na akatoa wito kwa wanaharakati wa haki za binadamu na vyombo vya habari kuendelea kutetea madai ya wananchi wa Bahrain kupitia uhamasishaji na njia halali za kisheria.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha